DALILI ZA HATARI KWA MAMA MJAMZITO🔥

1. Damu ukeni

Katika mazingira ya kawaida, damu huwa haipaswi kutoka wakati wote wa ujauzito.

Katika mazingira fulani, siku ya 10-14 baada ya kutungwa kwa ujauzito mwanamke anaweza kutokwa na damu kidogo ambayo humaanisha kuwa kijusi kinajishikiza kwenye mji wa uzazi ili kianze kulelewa. ( 1 )

Kutokwa na damu ukeni muda wowote mwingine siyo ishara nzuri hivyo inapawa kuchukuliwa kama jambo la dharura.

Baadhi ya sababu zinazoweza kufanya damu itoke ni uwepo wa maambukizi makubwa, tishio la kuharibika kwa ujauzito, kuwa na ujauzito unaolelewa nje ya mji wa uzazi au uwepo wa changamoto zozote kwenye kondo la uzazi. ( 2, 3 )

2. Kifafa na degedege

Shinikizo la juu la damu wakati wa ujauzito ambalo huambatana na uwepo wa protini kwenye mkojo husababisha kifafa cha ujauzito.

Hali hii ya kifafa na degedege huwa ni hatari kwa afya ya mama na mtoto.

Inaweza kusababisha kifo cha mama au mtoto, kuharibika kwa ujauzito, kujifungua kabla ya wakati, kuathiri mfumo wa fahamu, kuharibu viungo vya mwili, upofu pamoja na kujifungua watoto wenye tatizo la degedege.

3. Kichwa na macho

Maumivu makali ya kichwa na kupungua uwezo wa macho kwenye kuona ni dalili za kifafa cha ujauzito.

Ni muhimu sana kwa mwanamke mjamzito kufika hospitalini haraka.

Dalili hizi mara nyingi huonekana kuanzia wiki ya 20 ya ujauzito na kuendelea.

4. Mtoto kuacha kucheza

Baadhi ya watoto huanza kucheza kuanzia wiki ya 13-16 tangu mwanamke aone hedhi yake ya mwisho.

Kwa wanawake wenye ujauzito wa kwanza wanaweza kuchelewa hadi wiki ya 18-20 ndipo wahisi miondoko ya mtoto.

Kwa kuwa kila mwanamke hupata ujauzito kwa namna yake, wastani wa muda wa kawaida wa kuanza kucheza kwa mtoto huwa ni kuanzia wiki ya 13-25. ( 4 )

Kama mtoto alikuwa kazoea kucheza kisha akaacha ghalfa, unapaswa kuwa na wasiwasi maana hii siyo ishara nzuri.

Fika hospitalini kwa uchunguzi ili kufahamu kama tukio hili lina maana nzuri au mbaya.

5. Maumivu makali tumboni

Maumivu makali ya tumbo hasa yale yanayotokea kwenye sehemu ya chini ya tumbo huwa siyo mazuri.

Maumivu haya yanaweza kuambatana na hali ya kukaza kwa misuli ya tumbo.

Yanaweza kuwa na maana kuwa mwanamke anataka kupatwa na uchungu wa mapema kabla ya muda halisi.

Ni muhimu kufika hospitalini kwa uchunguzi na matibabu.

6. Kupasuka kwa chupa

Mtoto huhifadhiwa kwenye nyumba ya uzazi ambayo kwa lugha rahisi inayofahamika zaidi huitwa chupa ya uzazi.

Chupa hii haipaswi kupasuka muda wowote ule kabla ya uchungu wa kuzaa.

Wastani wa asilimia 3-10 ya wanawake wote wanaojifungua. ( 5 )

Kupasuka kwa chupa ya uzazi kabla ya siku sahihi ya uchungu husababisha maambukizi kwa mama na mtoto, kunyofoka kwa kondo la uzazi pamoja na changamoto kwenye kitovu.

Ni muhimu kufika hospitalini ili tiba sahihi iweze kutolewa. 

Inaweza kuhusisha matumizi ya dawa, sindano au kuzalishwa haraka ikiwa ujauzito utakuwa umefikia kwenye hatua ambayo mtoto akitolewa ataweza kuishi.

7. Homa kali

Kupanda kwa joto hadi 100.4°F (38°C) siyo jambo zuri kutokea wakati wa ujauzito.

Homa hii inaweza kuwa hatari zaidi kama itaambatana na kiungulia, kuhara, maumivu makali ya tumbo na mgongo, kupungua kwa mkojo pamoja na kutokwa na uchafu ukeni wenye rangi na hatufu kali.

Inaweza kuwa ishara ya uwepo wa maambukizi makali kwenye sehemu mbalimbali za mwili hasa zile zinazohusisha figo, mji wa uzazi au mapafu.

8. Maumivu ya kifua

Katika mazingira ya kawaida, maumivu ya kifua wakati wa ujauzito huwa hayana maana mbaya.

Husababishwa na kiungulia, au mgandamizo mkubwa unaofanywa na mtoto kwenye kusukuma viungo vya mwili kuelekea nafasi ya wazi ya kifua.

Hali inaweza isiwe ya kawaida kama maumivu haya ya kufua yataambatana na changamoto za kupumua pamoja na kuongezeka kwa mapigo ya moyo.

Uchunguzi wa haraka unahitajika.

9. Uvimbe

Kuvimba kwa mwili wakati wa ujauzito ni jambo la kawaida.

Uvimbe huu mara nyingi hutokea kwenye mikono, miguu, uso na maungio ya mifupa. ( 6 )

Hata hivyo, katika nyakati chache, kuvimba kwa mwili kunaweza kuwa dalili mbaya ya uwepo wa changamoto kubwa za kiafya hasa kifafa cha mimba.

Husababisha ongezeko kubwa la shinikizo la damu wakati wa ujauzito na wakati wa kujifungua.

Maana nyingine ya kutokea kwa uvimbe ni uwepo wa damu iliyoganda kwenye mishipa ya damu maarufu zaidi kama deep vein thrombosis (DVT).

Tatizo hili huathiri mzunguko wa damu mwilini. ( 7, 8 )

Ni muhimu upatikane uthibitisho wa daktari kuwa uvimbe husika hauna maana mbaya kwa afya.

Muhtasari

Hali ya ujauzito wa mwanamke mmoja huwa haifanani na mwingine.

Ni kosa kubwa sana kutumia uzoefu wa mwanamke mwingine kwenye kuchukua maamuzi yanayohusu afya yako.

Ukipata jambo lolote linalokupa wasiwasi fika hospitalini haraka.

KWA ELIMU ZAIDI JUU YA AFUA YA UZAZI KWA MWANAUME/MWANAMKE PAMOJA NA SAYANSI YA TENDO LA NDOA📲:+255746641655

Au bonyeza link hii kuja wattsap inbox👉https://bit.ly/3XgpzOD